Mwongozo wa Mwombaji wa Kazi Serikalini
Muhimu: Maombi yote ya kazi katika Utumishi wa Umma yanawasilishwa kupitia mfumo huu wa kielektroniki pekee. Maombi yatakayotumwa kwa njia ya posta au barua pepe hayatafanyiwa kazi.
1. Mahitaji ya Awali Kabla ya Kuomba
- Anwani ya barua pepe (Email) inayofanya kazi na unayoikumbuka nenosiri lake.
- Namba ya simu ya mkononi iliyosajiliwa kisheria.
- Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA).
- Nakala za kielektroniki (PDF, JPG au PNG) za vyeti vyako halisi, zikiwa safi na zinazosomeka vizuri (zisizozidi ukubwa wa 2MB kila moja).
2. Hatua za Kujaza Wasifu (Profile)
Baada ya kujisajili na kuthibitisha akaunti yako:
- Taarifa Binafsi: Weka majina yako kamili kama yanavyosomeka kwenye cheti chako cha kuzaliwa au cheti cha kidato cha nne.
- Vyeti vya Elimu: Anza na cheti cha Kidato cha Nne (CSEE), kisha Kidato cha Sita (kama unacho), na baada ya hapo vyeti vya Astashahada, Stashahada, au Shahada.
- Bodi za Kitaaluma: Kwa kada zinazodai usajili wa bodi (mfano: ERB, NBAA, PSPTB, TLS, MCT), lazima uweke namba ya usajili na upakie cheti cha bodi.
- Wadhamini (Referees): Weka angalau wadhamini wawili (2) na wasiozidi watano (5) wakiwemo waajiri wako wa zamani au wakufunzi wako chuoni.
3. Uteuzi na Usaili
Waombaji watakaokidhi vigezo watachujwa na kupewa alama. Orodha fupi (Shortlist) itawekwa wazi kwenye mfumo na barua rasmi za wito wa usaili zitapakuliwa kutoka kwenye akaunti ya kila mwombaji aliyeteuliwa.